Tangazo

Thursday, August 28, 2014

ETOO ASTAAFU SOKA KIMATAIFA

Etoo astaafu soka ya kimataifa
Mfungaji mabao mengi zaidi wa timu ya taifa ya Cameroon Samuel Eto'o ametangaza kustaafu soka ya kimataifa.
Mshambulizi huyo ambaye ameifungia Cameroon mabao 56 amejiunga na Everton ya Uingereza juzi .

Kufuatia kauli hiyo mshambulizi huyo sasa atakuwepo katika kipindi chote cha cha kombe la mataifa bingwa barani Afrika mwezi Januari mwakani.
"nataka kuwajuza kuwa nimestaafu mashindano yote ya kimataifa ''aliandika Etoo katika mtandao wake wa kijamii wa Instagram .
Mechi yake ya mwisho ilikuwa dhidi ya Mexico
"Ningependa kuwashukuru sana mashabiki wangu kote barani Afrika na duniani kwa mchango wao ."
Mshambulizi huyo wa zamani wa Barcelona, Inter na Real Madrid alicheza mechi yake ya kwanza ya kimataifa mwaka wa 1997 Cameroon iliponyeshewa 5-0 na Costa Rica.
Mechi yake ya mwisho ya kimataifa ilikuwa dhidi ya Mexico katika kombe la dunia huko Brazil.

Thursday, August 21, 2014

UKAWA WAPOTEZEWA



Katibu Mkuu wa CCM, Abrahman Kinana akitoa taarifa katika kikao cha Kamati Kuu ya chama hicho, mjini Dodoma juzi. Kushoto ni Makamu Mwenyekiti wa Zanzibar, Rais Ali Mohamed Shein, Rais Jakaya Kikwete na Makamu wa Tanzania Bara Phillip Mangula. Picha na Emmanuel Herman 



“Siyo lazima warejee bungeni maana hiyo siyo njia pekee ya kupatikana kwa suluhisho, kuna options (njia) nyingi za kufikia mwafaka na sisi tutazitumia hizo kwa sababu lengo letu ni kuhakikisha kwamba nchi yetu inaendelea kuwa katika hali ya usalama na amani,” alisema Kinana jana mjinihapa.
Katibu mkuu huyo alikuwa akijibu swali lililomtaka kueleza njia atakazotumia kusaka suluhu ya mchakato wa Katiba baina ya chama chake na vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), kama alivyoagizwa na Kamati Kuu (CC) ya CCM iliyofanyika juzi.
 
Kamati Kuu ilitoa agizo hilo baada ya kupokea taarifa tatu za mwenendo wa mchakato wa Katiba zilizowalishwa na Kinana, Katibu wa Siasa na Uhusiano wa Kimataifa wa CCM ambaye pia ni Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Asha-Rose Migiro na Katibu wa Wabunge wa CCM na Naibu Waziri Elimu naMafunzo ya Ufundi, Janister Mhagama
.

“Kuna njia mbili kubwa za kuendelea kusaka maridhiano; kwanza ni kupitia Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD) na Baraza la Vyama vya Siasa ambako kuna fursa za viongozi wa vyama kujadiliana masuala mbalimbali licha ya tofauti za mitizamo na itikadi za vyama vyetu,” alisema Kinana na kuongeza:

“Tumekuwa tukizungumza na kuna kila dalili ya kupata mwafaka licha ya kwamba siyo lazima mwafaka huo uwalazimishe waliotoka kurejea bungeni, lakini jambo la msingi lazima tuhakikishe mazingira ya kuendesha siasa zetu ni salama kwa faida ya vyama vyetu nchi yetu.

Alisema mbali na suala la kuwashawishi Ukawa warejee bungeni, majadiliano ya vyama vya siasa pia yanalenga kujadili jinsi ya kujenga mazingira sawa ya uendeshaji wa siasa, hasa katika kipindi hiki Taifa linapoelekea kwenye Uchaguzi Mkuu wa 2015.

Kinana alisema pamoja na kuvunjika kwa mazungumzo yaliyokuwa yakiratibiwa na Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi anaamini TCD ni sehemu mwafaka kwani inajumuisha viongozi wa vyama ambavyo siyo sehemu ya mvutano uliopo.

Taarifa za ndani

Kauli ya Kinana inashabihiana na habari kutoka ndani ya chama chake ambazo zimekuwa zikidai kwamba chama hicho tayari kimefanya mazungumzo na wapinzani kwa ajili ya kuifanyia marekebisho ya Katiba ya sasa ili kujenga mazingira ya usawa katika Uchaguzi Mkuu ujao
.

Tayari vyama vya upinzani vimependekeza mambo manne yanayopaswa kuzingatiwa katika mabadiliko hayo ambayo ni kuwapo kwa Tume Huru ya Uchaguzi, Matokeo ya urais kuhojiwa Mahakamani, kuruhusiwa kwa mgombea binafsi na mshindi wa urais kupata kura zaidi ya asilimia 50 tofauti na sasa.
Katika muktadha huo, ndiyo maana Ukawa wamekuwa na msimamo wa kutaka Bunge hilo lisitishwe kusubiri mwafaka, jambo ambalo hata hivyo, Kinana alisema ni ngumu kutekelezwa kwa sababu sheria imefunga milango kuhusu suala hilo

Wednesday, August 20, 2014

PAPA FRANCIS AJITABIRIA MAUTI


Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani, Papa Fransis. PICHA|MAKTABA 


Katika hali isiyo ya kawaida kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani, Papa Francis ametabiri ukomo wa maisha yake duniani akisema kuwa anaamini Mungu atampa miaka isiyozidi mitatu.

Akizungumza na waandishi wa habari kwenye ndege wakati akitoka ziarani Korea Kusini kurejea Vatican, Papa Francis alisema suala la kuendelea kuishi ni neema ya Mungu.

“Suala hili naliona kama neema tu ya Mungu kwa watu wake. Najaribu kutafakari kuhusu dhambi zangu na makosa yangu, siwezi kujivuna. Najua kwa sababu hali hii itadumu kwa muda mchache. Miaka miwili au mitatu nitakuwa nimeondoka na kwenda nyumbani kwa baba,” alisema.

Papa Francis (77), aliongeza kuwa anaweza kustaafu endapo atahisi kwamba afya yake hairuhusu kuendelea na kazi. Kuachia madaraka ndani ya kanisa katoliki kwa viongozi wanaohisi afya zao kuteteleka ambapo mwaka jana Papa Benedict XVI aliyeng’atuka kutokana na matatizo ya kiafya.

Pamoja na kwamba Papa Francis hajawahi kuzungumza hadharani kuhusu ni lini pengine anaweza kufariki dunia, lakini baadhi ya vyanzo vya habari kutoka Vatican vinasema kuwa kiongozi huyo amekuwa akiwaambia watu wake wa karibu kuhusu siku zake chache zilizosalia duniani.

Wachambuzi wa masuala ya kiimani kwa nyakati tofauti walisema huenda kiongozi huyo ana tatizo la kiafya ambalo halijawekwa wazi.

Wakati hayo yakiendelea taarifa za ndani zinabainisha kwamba kiongozi huyo aliwahi kutolewa pafu moja baada ya kuathirika wakati akiwa kijana nchini Argentina.

Source Mwananchi 

Tuesday, August 12, 2014

BBC YAZINDUA OFISI MPYA DAR

Wafanyakazi wa BBC wakiwa kazini kupeperusha matangazo ya Dira ya Dunia redio
Idhaa ya kiswahili ya BBC imezindua rasmi studio zake mjini Dar es Salaam kwa mbwembwe na haiba kuu.
Uzinduzi huo ni matokeo ya mkakati na uwekezaji wa miaka mingi wa shirika la BBC duniani kuhakikisha kuwa matangazo yake yanawafikia wasikilizaji katika hali ya ubora wa hali ya juu na ya kisasa zaidi. Katika hafla hiyo iliyoandaliwa katika ofisi hizo hizo mpya zilizoko eneo la Mikocheni, mkuu wa kitengo cha uandishi wa habari katika BBC, Nicki Clarke, ameshukuru serikali ya Tanzania, kwa kuwaruhusu kujenga studio hizo za kisasa zitakazoinua tasnia ya habari nchini humo na uhuru wa habari kwa ujumla.
Naye mkuu wa ofizi ya Dar es Salaam, Hassan Mhelela mbali na kuwataka wafanyakazi wa BBC Tanzania, kuzidi kuonyesha ushirikiano pamoja na utendaji kazi wa pamoja, pia ametangaza kuanishwa rasmi kwa ushirikiano kati ya BBC na chuo kikuu cha Dar es Salaam kitengo cha uandishi wa habari.

Eric David Nampesya akizipa taabu Tumba kwenye sherehe ya ufunguzi wa ofisi za BBC Dar es Salaam
Ushirikiano huo amesema kuwa unalenga kusaidia kutoa mafunzo kwa wandishi wa habari chipukizi walioko mafunzoni katika chuo hicho, ambao kwa nyakati tofauti, watakuwa wakijiunga na BBC ili kupata mafunzo katika uandaaji vipindi vya redio na televisheni pamoja na utangazaji.
Kwa upande wa BBC, kuanzishwa kwa ofisi hii, yenye studio za kisasa kabisa za redio na televisheni mbali na kuongeza ubora wa vipindi lakini pia kutawezesha matangazo ya redio na televisheni kufanyika moja kwa moja kutokea Dar es Salaam.

Na kuanzia sasa matangazo ya Amka na BBC yatakuwa yakiandaliwa Dar es Salaam.

Itakumbukwa kuwa Tanzania mbali na kuwa na wasikilizaji wengi wa idhaa ya kiswahili ya BBC, lakini pia ndiko kunakozungumzwa zaidi lugha ya kiswahili.

Tanzania pia ina rekodi ambapo mtangazaji wa kwanza au sauti ya kwanza iliyosikika mwaka 1957, ilikuwa ya mtanzania Oscar Kambona ambapo alikuwa mwanafunzi mjini London.

Bunge Maalumu mtegoni tena kuanzia leo

Mwenyekiti wa Bunge Maalum la Katiba,Samuel Sitta. PICHA |MAKTABA 
Mjadala kuhusu masuala ya Muungano unatarajiwa kurejea upya katika kamati za Bunge Maalumu leo, wakati zitakapoanza kujadili sura za saba, nane, kumi na moja, 18 na 15 za Rasimu ya Katiba.Kamati zimepewa siku sita kujadili sura hizo tano ambazo zina jumla ya ibara 79, huku miongoni mwake zikigusa masuala mengi ambayo msingi wake umejengwa juu ya mfumo wa serikali tatu.
Miongoni mwa masuala hayo ni pamoja na baraza la mawaziri, tume ya kusimamia na kuratibu uhusiano baina ya Serikali ya Muungano na Serikali za Nchi Washirika (Tanganyika na Zanzibar), Sekretarieti ya Tume ya Uhusiano na Uratibu, Masuala yanayohusu Benki Kuu na Fedha pamoja na uteuzi wa watumishi katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Suala la aina ya muungano lilianza kujadiliwa katika sura ya kwanza na ya sita katika awamu ya kwanza ya Bunge iliyomalizika mwishoni mwa Aprili mwaka huu na kuzua mvutano mkali ambao hatimaye ulisababisha baadhi ya wajumbe wa Bunge Maalumu kususia mchakato huo.Wajumbe hao ni wale wanaotokana na vyama vya siasa vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) ambao wanataka mapendekezo yaliyomo kwenye Rasimu ya Katiba ya kuwapo kwa muundo wa serikali tatu yabaki kama yalivyo na upande mwingine unaowajumuisha wabunge wengi wa CCM ukitaka muundo wa sasa wa Serikali mbili uendelee.

Kutokana na mvutano huo, Bunge Maalumu liliahirisha upigaji kura kuamua aina ya muundo unaofaa, lakini hata liliporejea Agosti 5, mwaka huu halikuweza kupiga kura, badala yake lilibadilisha kanuni ili kuwezesha upigaji kura kufanyika baada ya kumaliza mjadala wa sura zote ndani ya kamati. 

Katibu wa Bunge Maalumu, Yahya Khamis Hamad alisema hakuna maelekezo yoyote yaliyotolewa kwa wajumbe kuhusu jinsi ya kujadili masuala yanayohusu muungano na kwamba wajumbe watazingatia mapendekezo waliyoyatoa katika rasimu ya kwanza na ya sita.“Sidhani kama ni wajibu wetu kutoa maelekezo yoyote, kinachoweza kutokea ni wajumbe kuzingatia kila walichokijadili na kukubaliana katika sura zile za awali, kama walikubali serikali ya shirikisho watazingatia hilo, kama walikubaliana serikali mbili watazingatia hilo pia,” alisema Hamad.

Itakumbukwa kwamba idadi kubwa ya kamati baada ya kujadili sura ya kwanza na ya sita zinazohusu aina ya muungano, zilipendekeza kuachana na muundo wa shirikisho na kuwasilisha maoni yanayotaka kuendelea kwa mfumo wa Serikali mbili. 

Kamati nyingi zilipata idadi ya kura za kutosha kuunga mkono mapendekezo hayo na chache zilikosa theluthi mbili kutoka kwa wajumbe wa Tanzania Bara na Zanzibar.

Ikiwa kamati hizo zitazingatia uamuzi wake wa awali, basi masuala yote yanayogusa serikali tatu yatafutwa, hivyo zitakuwa na kazi kubwa ya kuandika upya ibara nyingi zinazozingatia utekelezaji wa mfumo serikali mbili.
Maudhui ya Ibara
Ibara ya 98 ya Rasimu pamoja na mambo mengine, inazungumzia idadi ya mawaziri ambao idadi yao hawapaswi kuzidi 15, huku uteuzi wao ukipendekezwa uthibitishwe na Bunge.

Monday, August 4, 2014

WAZIRI MKUU MH. MIZENGO PINDA AITAKA TAASISI YA KILIMO CHA MBOGA MBOGA KUONGEZA JUHUDI KATIKA KUTOA ELIMU KWA WAKULIMA.

Mkurugenzi mtendaji wa TAHA, Jackline Mkindi akiwaeleza wadau wa Kilimo waliohudhuria kuwa ni muda mrefu kilimo cha  mazao ya Maua, Matunda, mboga mboga, viungo, mbegu na viazi kimesahaulika na kwamba ni kilimo kinachoweza kumkomboa mkuilima kutokana na urahisi wa ulimaji wake aliwasisitiza waendeleze Kilimo hicho.
Meza Kuu 
Wadau Mbalimbali waliohudhuria katika Mkutano huo

WAZIRI Mkuu wa Tanzania, Mizengo Pinda ameitaka taasisi ya Kilimo cha mbogamboga(Tanzania Horticultural Association)TAHA kuongeza juhudi za kutoa elimu kwa wakulima.
Rai hiyo aliitoa juzi katika kongamano la Uwekezaji lililofanyika katika ukumbi wa Mkapa jijini Mbeya ambapo alikuwa mwenyekiti wa kongamano hilo.
Waziri Mkuu mbalo na kuwataka TAHA kuongeza juhudi pia alisifu juhudi zao katika kuinua kilimo na matumizi ya fursa za uwekezaji kwa wakulima.
Akizungumza katika Kongamano hilo, Mkurugenzi mtendaji wa TAHA, Jackline Mkindi, aliwaambia wadau wa Kilimo waliohudhuria kuwa ni muda mrefu kilimo cha  mazao ya Maua, Matunda, mboga mboga, viungo, mbegu na viazi kimesahaulika na kwamba ni kilimo kinachoweza kumkomboa mkuilima kutokana na urahisi wa ulimaji wake.
Alisema wakulima inabidi waelimishwe kuhusu kilimo cha mazao hayo kwa sababu hakihitaji maeneo makubwa na mtaji wa kutosha bali hulimwa katika eneo dogo lakini yakilenga soko la nje na sio kulima kwa mazoea kwa ajili ya matumizi ya nyumbani.
Alisema ili kilimo cha mazao hayo kiwe na manufaa kwa wakulima wa Nyanda za Juu kusini na kukidhi mahitaji ya soko la nje inabidi serikali iangalie Changamoto zianazovikabili viwanja vingine vya ndege katika usafirishaji wa mazao hayo kama Uwanja wa Kilimanjaro( KIA) na Dar Es Salaam( JIA).
Mkurugenzi huyo alisema maeneo yanayopaswa kuangaliwa mapema kabla ya kuanza kwa kilimo cha mazao hayo kwa Uwanja wa Kimataifa wa Songwe ni pamoja na uwepo wa Ndege kubwa ya kusafirisha mizigo inayoweza kupeleka bidhaa hizo moja kwa moja sokoni pasipo kuathiriwa.
Aliyataja maeneo mengine kuwa ni kuwepo kwa eneo kubwa na jengo karibu na Uwanja wa Ndege kwa ajili ya kupozea mazao hayo ili yasiharibike na sehemu maalumu ya kushushia mazao hayo na kupakilia kwenye ndege pasipo kuyabughudhi na kuyaharibu kabla ya kufika sokoni.
Alisema kutokuwepo kwa vitu hivyo kunapunguza ubora wa bidhaa hizo kama maua ambayo hayatakiwi kunyauka hadi yanafikishwa sokoni ndipo yanakuwa na soko la uhakika nje ya nchi.
Aliongeza kuwa soko la nje ya mazao hayo lipo na linauhitaji mkubwa isipokuwa ni kuzingatia vigezo vya usafirishaji ili kuyafanya yafike sokoni kama yalivyotolewa shambani.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Abbasi Kandoro alisema lengo la mafunzo hayo ni kujadili namna ya kuwawezesha wananchi kujikita katika uzalishaji wa mazao ya matunda, mboga mboga na maua  ili waweze kuboresha vipato vyao.
Alisema pia ni utekelezaji wa agizo la Raisi kuhusu manufaa ya uwanja wa Ndege kwa kilimo hicho kwa Mikoa ya Nyanda za Juu Kusini, ambapo aliwataka viongozi wenzie kutekeleza kwa vitendo agizo hilo na siyo kuiongea tu mdomoni.