Tangazo

Wednesday, August 20, 2014

PAPA FRANCIS AJITABIRIA MAUTI


Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani, Papa Fransis. PICHA|MAKTABA 


Katika hali isiyo ya kawaida kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani, Papa Francis ametabiri ukomo wa maisha yake duniani akisema kuwa anaamini Mungu atampa miaka isiyozidi mitatu.

Akizungumza na waandishi wa habari kwenye ndege wakati akitoka ziarani Korea Kusini kurejea Vatican, Papa Francis alisema suala la kuendelea kuishi ni neema ya Mungu.

“Suala hili naliona kama neema tu ya Mungu kwa watu wake. Najaribu kutafakari kuhusu dhambi zangu na makosa yangu, siwezi kujivuna. Najua kwa sababu hali hii itadumu kwa muda mchache. Miaka miwili au mitatu nitakuwa nimeondoka na kwenda nyumbani kwa baba,” alisema.

Papa Francis (77), aliongeza kuwa anaweza kustaafu endapo atahisi kwamba afya yake hairuhusu kuendelea na kazi. Kuachia madaraka ndani ya kanisa katoliki kwa viongozi wanaohisi afya zao kuteteleka ambapo mwaka jana Papa Benedict XVI aliyeng’atuka kutokana na matatizo ya kiafya.

Pamoja na kwamba Papa Francis hajawahi kuzungumza hadharani kuhusu ni lini pengine anaweza kufariki dunia, lakini baadhi ya vyanzo vya habari kutoka Vatican vinasema kuwa kiongozi huyo amekuwa akiwaambia watu wake wa karibu kuhusu siku zake chache zilizosalia duniani.

Wachambuzi wa masuala ya kiimani kwa nyakati tofauti walisema huenda kiongozi huyo ana tatizo la kiafya ambalo halijawekwa wazi.

Wakati hayo yakiendelea taarifa za ndani zinabainisha kwamba kiongozi huyo aliwahi kutolewa pafu moja baada ya kuathirika wakati akiwa kijana nchini Argentina.

Source Mwananchi 

No comments:

Post a Comment