Tangazo

Monday, August 4, 2014

WAZIRI MKUU MH. MIZENGO PINDA AITAKA TAASISI YA KILIMO CHA MBOGA MBOGA KUONGEZA JUHUDI KATIKA KUTOA ELIMU KWA WAKULIMA.

Mkurugenzi mtendaji wa TAHA, Jackline Mkindi akiwaeleza wadau wa Kilimo waliohudhuria kuwa ni muda mrefu kilimo cha  mazao ya Maua, Matunda, mboga mboga, viungo, mbegu na viazi kimesahaulika na kwamba ni kilimo kinachoweza kumkomboa mkuilima kutokana na urahisi wa ulimaji wake aliwasisitiza waendeleze Kilimo hicho.
Meza Kuu 
Wadau Mbalimbali waliohudhuria katika Mkutano huo

WAZIRI Mkuu wa Tanzania, Mizengo Pinda ameitaka taasisi ya Kilimo cha mbogamboga(Tanzania Horticultural Association)TAHA kuongeza juhudi za kutoa elimu kwa wakulima.
Rai hiyo aliitoa juzi katika kongamano la Uwekezaji lililofanyika katika ukumbi wa Mkapa jijini Mbeya ambapo alikuwa mwenyekiti wa kongamano hilo.
Waziri Mkuu mbalo na kuwataka TAHA kuongeza juhudi pia alisifu juhudi zao katika kuinua kilimo na matumizi ya fursa za uwekezaji kwa wakulima.
Akizungumza katika Kongamano hilo, Mkurugenzi mtendaji wa TAHA, Jackline Mkindi, aliwaambia wadau wa Kilimo waliohudhuria kuwa ni muda mrefu kilimo cha  mazao ya Maua, Matunda, mboga mboga, viungo, mbegu na viazi kimesahaulika na kwamba ni kilimo kinachoweza kumkomboa mkuilima kutokana na urahisi wa ulimaji wake.
Alisema wakulima inabidi waelimishwe kuhusu kilimo cha mazao hayo kwa sababu hakihitaji maeneo makubwa na mtaji wa kutosha bali hulimwa katika eneo dogo lakini yakilenga soko la nje na sio kulima kwa mazoea kwa ajili ya matumizi ya nyumbani.
Alisema ili kilimo cha mazao hayo kiwe na manufaa kwa wakulima wa Nyanda za Juu kusini na kukidhi mahitaji ya soko la nje inabidi serikali iangalie Changamoto zianazovikabili viwanja vingine vya ndege katika usafirishaji wa mazao hayo kama Uwanja wa Kilimanjaro( KIA) na Dar Es Salaam( JIA).
Mkurugenzi huyo alisema maeneo yanayopaswa kuangaliwa mapema kabla ya kuanza kwa kilimo cha mazao hayo kwa Uwanja wa Kimataifa wa Songwe ni pamoja na uwepo wa Ndege kubwa ya kusafirisha mizigo inayoweza kupeleka bidhaa hizo moja kwa moja sokoni pasipo kuathiriwa.
Aliyataja maeneo mengine kuwa ni kuwepo kwa eneo kubwa na jengo karibu na Uwanja wa Ndege kwa ajili ya kupozea mazao hayo ili yasiharibike na sehemu maalumu ya kushushia mazao hayo na kupakilia kwenye ndege pasipo kuyabughudhi na kuyaharibu kabla ya kufika sokoni.
Alisema kutokuwepo kwa vitu hivyo kunapunguza ubora wa bidhaa hizo kama maua ambayo hayatakiwi kunyauka hadi yanafikishwa sokoni ndipo yanakuwa na soko la uhakika nje ya nchi.
Aliongeza kuwa soko la nje ya mazao hayo lipo na linauhitaji mkubwa isipokuwa ni kuzingatia vigezo vya usafirishaji ili kuyafanya yafike sokoni kama yalivyotolewa shambani.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Abbasi Kandoro alisema lengo la mafunzo hayo ni kujadili namna ya kuwawezesha wananchi kujikita katika uzalishaji wa mazao ya matunda, mboga mboga na maua  ili waweze kuboresha vipato vyao.
Alisema pia ni utekelezaji wa agizo la Raisi kuhusu manufaa ya uwanja wa Ndege kwa kilimo hicho kwa Mikoa ya Nyanda za Juu Kusini, ambapo aliwataka viongozi wenzie kutekeleza kwa vitendo agizo hilo na siyo kuiongea tu mdomoni.

No comments:

Post a Comment