Mwenyekiti wa Bunge Maalum la Katiba,Samuel Sitta. PICHA |MAKTABA
Mjadala kuhusu masuala
ya Muungano unatarajiwa kurejea upya katika kamati za Bunge Maalumu leo,
wakati zitakapoanza kujadili sura za saba, nane, kumi na moja, 18 na 15
za Rasimu ya Katiba.Kamati zimepewa siku sita kujadili sura hizo tano
ambazo zina jumla ya ibara 79, huku miongoni mwake zikigusa masuala
mengi ambayo msingi wake umejengwa juu ya mfumo wa serikali tatu.
Miongoni mwa masuala hayo ni pamoja na baraza la
mawaziri, tume ya kusimamia na kuratibu uhusiano baina ya Serikali ya
Muungano na Serikali za Nchi Washirika (Tanganyika na Zanzibar),
Sekretarieti ya Tume ya Uhusiano na Uratibu, Masuala yanayohusu Benki
Kuu na Fedha pamoja na uteuzi wa watumishi katika Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania.
Suala la aina ya muungano lilianza kujadiliwa
katika sura ya kwanza na ya sita katika awamu ya kwanza ya Bunge
iliyomalizika mwishoni mwa Aprili mwaka huu na kuzua mvutano mkali ambao
hatimaye ulisababisha baadhi ya wajumbe wa Bunge Maalumu kususia
mchakato huo.Wajumbe hao ni wale wanaotokana na vyama vya siasa
vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) ambao wanataka
mapendekezo yaliyomo kwenye Rasimu ya Katiba ya kuwapo kwa muundo wa
serikali tatu yabaki kama yalivyo na upande mwingine unaowajumuisha
wabunge wengi wa CCM ukitaka muundo wa sasa wa Serikali mbili uendelee.
Kutokana na mvutano huo, Bunge Maalumu
liliahirisha upigaji kura kuamua aina ya muundo unaofaa, lakini hata
liliporejea Agosti 5, mwaka huu halikuweza kupiga kura, badala yake
lilibadilisha kanuni ili kuwezesha upigaji kura kufanyika baada ya
kumaliza mjadala wa sura zote ndani ya kamati.
Katibu wa Bunge Maalumu, Yahya Khamis Hamad
alisema hakuna maelekezo yoyote yaliyotolewa kwa wajumbe kuhusu jinsi ya
kujadili masuala yanayohusu muungano na kwamba wajumbe watazingatia
mapendekezo waliyoyatoa katika rasimu ya kwanza na ya sita.“Sidhani kama ni wajibu wetu kutoa maelekezo
yoyote, kinachoweza kutokea ni wajumbe kuzingatia kila walichokijadili
na kukubaliana katika sura zile za awali, kama walikubali serikali ya
shirikisho watazingatia hilo, kama walikubaliana serikali mbili
watazingatia hilo pia,” alisema Hamad.
Itakumbukwa kwamba idadi kubwa ya kamati baada ya
kujadili sura ya kwanza na ya sita zinazohusu aina ya muungano,
zilipendekeza kuachana na muundo wa shirikisho na kuwasilisha maoni
yanayotaka kuendelea kwa mfumo wa Serikali mbili.
Kamati nyingi zilipata
idadi ya kura za kutosha kuunga mkono mapendekezo hayo na chache
zilikosa theluthi mbili kutoka kwa wajumbe wa Tanzania Bara na Zanzibar.
Ikiwa kamati hizo zitazingatia uamuzi wake wa
awali, basi masuala yote yanayogusa serikali tatu yatafutwa, hivyo
zitakuwa na kazi kubwa ya kuandika upya ibara nyingi zinazozingatia
utekelezaji wa mfumo serikali mbili.
Maudhui ya Ibara
Ibara ya 98 ya Rasimu pamoja na mambo mengine,
inazungumzia idadi ya mawaziri ambao idadi yao hawapaswi kuzidi 15, huku
uteuzi wao ukipendekezwa uthibitishwe na Bunge.
No comments:
Post a Comment